HISTORIA FUPI
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliunda Wizara ya Kuimarisha Viwango vya Raia na Haki za Wafanyakazi. Katika Wizara hiyo huduma Ustawi wa Jamii zilianzishwa na kutolewa fedha kwa jamii za Watu walio katika mazingira magumu. Huduma nyengine zilizotolewa ni pamoja hifadhi ya Wazee walio katika mazingira magumu, malipo ya pensheni ya kila mwezi na kiinua mgongo kwa wastaafu pamoja na fidia kwa wafanyakazi.
Mwaka 1967, masuala ya Ustawi wa Jamii yalihamishiwa Wizara ya Afya na kuundwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara hiyo iliendelea na Majukumu yake yakiwemo ya kutoa misaada kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu, fidia za wafanyakazi na kuanzisha Makazi ya Wazee Sebleni. Na baadae ya hapo Wizara kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii ilianzisha Makaazi ya wazee Welezo ambayo yalikuwa chini ya Wizara ya Afya kama hospitali maalum na kituo cha wagonjwa wa ukoma.
Mwaka 1983, mageuzi makubwa ya Wizara Zanzibar yalifanyika na Wizara mpya ya Kazi, Nguvu Kazi na Ustawi wa Jamii ilianzishwa, ikiwa na majukumu ya kutoa huduma za ustawi wa jamii Zanzibar pamoja na kusimamia kituo cha watoto yatima ambacho awali kilikuwa chini ya Wizara ya Elimu na Kituo cha kuwarekebisha watoto cha Tunguu kilianzishwa na kusimamiwa na Idara ya Ustawi wa Jamii. Kituo hicho kilitoa huduma za kuwarekebisha Tabia watoto watukutu na wale wanaokwenda na kinyume na sheria.
Mnamo mwezi Februari 1984, masuala yanayohusiana Ustawi wa Jamii ilihamishwa Ofisi ya Waziri Kiongozi na kupewa Majukumu ya ziada yakiwemo ya kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na utoaji wa viungo bandia, miwani, viti vya magurudumu na msaada wa elimu maalum kwa walemavu. Kituo cha kurekebisha tabia za walemavu kimeibuka katika kituo cha Forordhani Children’s Home ambacho kinahudumia watu wasioona na wenye ulemavu wa viungo. Kituo hicho kilitoa mafunzo kwa wanafunzi wasioona miongoni mwa mafunzo hayo ni kushona, kusuka, kutengeneza mikeka na shughuli mbali mbali za kujitegemea. Huduma nyingine zilikuwa zikitolewa kupitia Idara ya ustawi wa Jamii ni kusaidia akina mama wenye watoto watatu, kusaidia watu maskini kuanzisha biashara ndogo ndogo na malezi ya watoto waliotelekezwa.
Mwaka 1987, Shughuli za Ustawi wa Jamii zilirejea Wizara ya Afya na kuendelea na majukumu yake kwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazee kupitia mradi Help Age International. Mradi huo pamoja na mambo mengine ulihusisha utoaji wa msaada wa fedha kwa wazee vijijini kwa kila baada ya miezi mitatu kwa kusaidia katika matibabu, ujenzi wa nyumba na vyoo vya wazee na kuunda vikundi vya wazee katika maeneo mbali mbali kama vile Kivunge, Pwani Mchangani, Dole na Mkwajuni. Aidha Kufuatia Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake uliofanyika Beijing, Serikali ikaanzisha Sehemu ya Maendeleo ya Wanawake ilianzishwa katika Idara ya Ustawi wa Jamii. ambayo baadaye ikawa Wizara huru ya Wanawake na Watoto.
Mwaka 2004, huduma za Idara ziliimarishwa na huduma nyengine za watoto zilianzishwa kwa watu wenye ulemavu na usimamizi wa maafa zilihamishiwa katika idara zinazohusika baada ya kuanzishwa kwa Idara ya Watu wenye Ulemavu na Idara ya Usimamizi wa Maafa. mwaka wa 2009 huduma za Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto (CPU) na Huduma za Watoto Walio Katika Mazingira Hatarishi Zaidi (MVC) zilianzishwa ili kupiga vita aina zote za unyanyasaji na unyonyaji wa watoto na kuchukuwa hatua.
Mnamo Desemba 2010, DSW ilihamishwa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufuatia kuanzishwa kwa Wizara mpya ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto. Kituo cha Pamoja na Kitengo cha Ulinzi wa Jamii vilianzishwa sambamba na mchakato wa kuunda sera ya ulinzi wa jamii.
Mwaka 2014 Serikali ya Awamu ya Saba iliunda Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto iliundwa na Idara ya Ustawi wa Jamii ikiwa ni moja ya idara zake kuu. Kufuatia uchaguzi Mkuu wa Serikali, Serikali ya Awamu ya nane ya SMZ iliiunda Wizara Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto mwezi, disemba 2021, Wizara ambayo ilidumu kwa kipindi cha mwaka mmoja na hatimaye kuanzishwa rasmin Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeundwa. Lengo Kuu la kuundwa kwa Wizara hii ni Kuimarisha utoaji wa huduma bora za ustawi wa jamii, ulinzi kwa watu masikini katika jamii.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni miongoni mwa Wizara kumi na nane (18) za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika awamu ya nane inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi iliyoundwa tarehe 8 Machi, 2022.
Wizara ina jumla ya wafanyakazi 278 (Unguja 238 na Pemba 40) na imeundwa na Idara nne (4) na Ofisi Kuu Pemba, ambazo ni:
1. Idara ya Mipango, sera na Utumishi. (divisheni ya ufuatiliaji na tathmini, maendeleo ya sera, Mipango ya Kisekta na divisheni ya Utafiti).
2. Idara ya Uendeshaji na utumishi (divisheni ya Utumishi, Uendeshaji na divisheni ya Utunzaji Kumbukumbu).
3. Idara ya Ustawi wa jamii na Wazee. (divisheni ya hifadhi ya Mtoto, ustawi wa jamii, Pencheni jamii na divisheni ya maendeleo ya Wazee)
4. Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto (divisheni ya Jinsia, maendeleo ya jamii, Maendeleo ya Watoto na divisheni ya Uratibu wa mapambano ya vitendo vya ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.
5. Ofisi Kuu Pemba.