Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Siti Abasi Ali awataka Viongozi wa Dini kutumia nafasi zao katika kuielimisha jamii kuachana na vitendo viovu ili nchi ibaki salama.

Posted on: 03.01.2024

Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Siti Abasi Ali amewataka Viongozi wa Dini kutumia nafasi zao katika kuielimisha jamii kuachana na vitendo viovu ili nchi ibaki salama.

Akifungua kikao kazi cha Viongozi wa Dini huko Sebleni Wilaya ya Mjini amesema Viongozi wa Dini ni Watu muhimu hivyo wanapaswa  kuungana katika kupiga vita viendo hivyo.

Amesema lengo la kukutana na viongozi wa Dini ni kuweza kubadilishana mawazo na kuweka mikakati madhubuti, itakayoweza kuondosha viovu ambavyo vinaleta athari kwa jamii.

Aidha amesema Idara itahakikisha inakutana na Viongozi wa dini mara kwa mara ili kuweza kukumbushana na kuweza kutekeleza kwa ufanisi majukumu mbalimbali waliojipangia. 

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Viongozi wa Dini wa harakati Mwazini Jogoo ameahidi  kushirikiana na Idara ya maendeleo ya jamii,  jinsia na watoto ili waweze kufikia malengo yaliopangwa na Serikali katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji.

Amesema lengo ni kuhakikisha wanatoa elimu ya udhalilishaji katika jamii ili waweze kukemea vitendo hivyo.

Mapema Viongozi hao wa Dini wamesema wanatoa elimu  ya udhalilishaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Madrsa, Miskiti na Makanisa lakini wanapata ugumu kutoa elimu katika maeneo ya Skuli na Masheha.

Hivyo wameiomba Idara ya maenendeleo ya jamii, jinsia na Watoto  kukaa pamoja na wahusika hao ili kuweza kutoa elimu hiyo kwa ufanisi.

Wameeleza kuwa miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na mahudhurio madogo ya ya Wananchi katika mikutano , uhaba wa vitendea kazi na uhaba wa fedha za kuendeshea miradi wanayoianzisha katika shehia.

Hata hivyo wameomba kukutana mara kwa mara na Viongozi ili kuweza kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza katuka shehia zao.