Wanawake Tanzania wawezeshwa manunuzi ya umma kielektroniki
Posted on: 26.03.2024
Na Salma Lusangi New York
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imesema imewawezesha wanawake
kupata fursa za manunuzi ya umma kwa kutoa mafunzo ya kiufundi ili kuongeza
uwezo wa zabuni na matumizi bora ya mifumo ya ununuzi wa kielektroniki.
Taarifa hiyo imetolewa na
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma
mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifunga kikao cha pembeni (side Event) huko
New York, Nchini Marekani katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa.
Mhe Riziki amesema Serikali
imefanya juhudi hiyo ili kuwezesha kila raia wa
Tanzania kumudu faida sawa kutokana na fursa za manunuzi, hasa zile
zinazohusiana na biashara ndogo ndogo zinazoendeshwa na kumilikiwa na wanawake.
Amefahamisha kwamba jitihada hiyo inafanywa na Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
(PPRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs).
Alieleza Serikali
yaTanzania inasisitiza matumizi ya mfumo wa kitaifa wa ununuzi wa kielektroniki
ili kuweka mazingira mazuri ambayo pia yanaiwezesha Serikali kufuatilia idadi
ya mikataba ya manunuzi inayotolewa kwa wanawake.
Pia alisema ili kuhakikisha wanawake wanawezeshwa na ujuzi mdogo wa lugha ya Kiingereza, Serikali inatayarisha na kuhakikisha nyaraka za zabuni zimeandikwa katika Lugha yetu ya Taifa (Kiswahili) ili ziweze kueleweka kwa urahisi na kunufaisha makundi maalum fursa za manunuzi.
Mhe Riziki alifahamisha kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza safari ya ubunifu wa kuendeleza Dira yake mpya ya Maendeleo 2050 itakayoendesha Ajenda ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo ili kuhakikisha maono yanafafanuliwa vyema na mienendo ya kijamii na kiuchumi pamoja na mitazamo ya kijinsia, itazingatiwa.
“Safari ya ubunifu wa
kuendeleza Dira yake mpya ya Maendeleo 2050 itakayoendesha Ajenda ya Maendeleo
ya Taifa kwa miaka 25 itasaidia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na
wasichana katika mipango ya maendeleo ya kitaifa “ Alisema Pembe.
Aidha waziri huyo ametoa shukrani
za pekee kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali, maafisa wa Umoja wa Mataifa, Taasisi
za Utafiti na wadau wa elimu juu, sekta binafsi na vyombo vya habari kwa kufanikisha
mkutano huo.
Mapema akifungua kikao
hicho Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu
Hassan katika masuala ya Wanawake na Makundi Maalum Bi Sophia Mjema alisema
Tanzania Bara na Zanzibar, imeandaa sera, mikakati, mipango, na programu kadhaa
za kuwawezesha wanawake na wasichana na
kuhakikisha usawa wa kijinsia katika shughuli mbali mbali.
Alielezea Sera ya Taifa
ya Biashara ya mwaka 2003 imetaja haja
ya "kuunga mkono ushirikishwaji wa wanawake katika michakato ya maendeleo
ya biashara kupitia upatikanaji wa usawa zaidi wa mali za uzalishaji, hasa
ardhi yenye hati miliki, miundombinu, fedha, elimu na ujuzi".
Pia, kuongeza mafunzo na
kurekebisha taratibu za uendeshaji ili kuruhusu na kukuza matumizi ya mfumo wa
manunuzi ya umma; kushughulikia vikwazo vya kifedha na upatikanaji wa taarifa
za manunuzi ya umma.
Mkutano wa Hadhi ya Wanawake
(CSW68) ulianza tarehe 11 hadi 22 Machi
2024, New York nchini Marekani ambapo ya kikao cha pembeni kilikuwa na mada
isemayo Kufadhili Usawa wa kijinsia: Kuwawezesha Wanawake na Wasichana Kupata
Huduma za Umma na Kuendeleza Ahadi za Kizazi chenye Usawa nchini Tanzania.