Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma alitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kuharakisha masuala ya upelelezi kwa kesi za vitendo vya ukatili na udhalilishaji ili kuona zinamaliza ndani ya muda mfupi.

Posted on: 11.12.2023

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amelitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kuharakisha masuala ya upelelezi kwa kesi za vitendo vya ukatili na udhalilishaji ili kuona zinamaliza ndani ya muda mfupi.

Kauli hiyo aliitoa jana katika kilele cha maadhimisho ya kufunga siku 16 za harakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyofanyika katika kijiji cha Muyuni Wilaya ya Kusini Unguja.

Mhe. Riziki alisema taarifa za Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha hali inatisha kwani katika kipindi cha mwezi Januari hadi Octoba 2023 jumla ya matukio 1,620 yameripotiwa ambapo matukio 1,360 yanahusu watoto, 194 wanawake  na wanaume 77.

Alisema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi lakini bado ucheleweshwaji wa upelelezi wa matukio hayo umekuwa mkubwa hali ambayo inapelekea kesi nyingi kukaa muda mrefu katika vituo vya Polisi Zanzibar.

Alisema kuendelea kwa hali hiyo itaweza kuathiri malengo ya Serikali katika  mapambano ya kuondoa vitendo hivyo pamoja na kuwatia hatiani watu  wanaothibitika kutenda vitendo vya ukatili na kudhalilisha ndani ya nchi.

Aidha alisema ipo haja ya kutambua na kuweka kampeni maalum za kuyakabili matendo ya udhalilishaji wa Kijinsia kwa kuweka nguvu kazi na kampeni isemayo “Wekeza katika Kuzuwia Ukatili Dhidi ya Watu Wenye Ulemavu” na “Nijuze Nijilinde Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia”.

Alieleza kwamba kundi hilo la watu wenye ulemavu limekuwa na changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikiwakabili hivyo haja ya tafakuri ya kina inahitajika katika kumkomboa mtu mwenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, bi Abeida Rashid Abdalla, alisema bado matukio ya udhalilishaji yanaongezeka ikiwemo matukio ya kubaka, kunajisi ambapo Wilaya ya Mjini na Magharibi ‘A’ na ‘B’ zinaongoza kwa kesi nyingi.

Alieleza kwamba wakiwa wanahitimisha kilele cha siku 16 lakini bado mapambano yanaendelea hivyo ni lazima jamii kwa pamoja wanaumme na wanawake wote wanalazimika kupambana na matendo hayo kwani bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha matendo hayo yanaondoka nchini.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kusini Unguja, bi Radhia Rashid Haroub, aliipongeza Wizara hiyo kwa kuadhimisha siku 16 za kupinga vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji katika mkoa huyo. Alisema  bado nguvu za mapambano zinahitajika kwani Mkoa wa Kusini matukio hayo yameongezeka mwaka jana 2022 kulikua na jumla ya matukio 1,320 ambapo kwa mwaka huu yamefikia matukio 1,620 sawa na ongezeko la asilimia 16.

Kwa upande wa wanaharakati wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji akizungumza kwaniaba bi Amina Yussuf Ramadhani alisema jamii wameshapata uwelewa wa kuripoti vitendo hivyo lakini bado tatizo la muhali linaendelea kujitokeza na kusababisha baadhi ya kesi kusuluhishwa katika ngazi ya familia.